Wizara Ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida

SUWASA IMEWAKAMATA WATUHUMIWA WAWILI WA WIZI WA MITA ZA MAJI


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) imewakamata watuhumiwa 2 wa wizi wa mita za maji, wanaotambulika kwa majina ya Faraja Abel na Ayubu Shabani.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika eneo la Minga Mtaa wa Arusha road, wakiwa na Mita moja ya Maji iliyoharibiwa.

SUWASA ilipokea taarifa ya kukamatwa kwa watu hao kutoka kwa raia wema na kwa kushirikiana na Jeshi la polisi walifika katika eneo la tukio na kuwakamata.

Watuhumiwa hao wamefikishwa katika kituo kikuu cha polisi Singida Manispaa, kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi zaidi juu ya uharibifu mkubwa wa miundombinu uliofanyika.

Katika Sheria ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019 adhabu ya Makosa ya uharibifu wa miundombinu ya maji ni faini hadi shilingi milioni 50 au kifungo hadi miaka mitano.

SUWASA inawatahadharisha wale wote wanaojihusisha uharibifu huu wa Mali za Umma kuacha mara moja kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.