Wizara Ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida

KATIBU TAWALA WA MKOA WA SINGIDA ATEMBELEA MRADI WA MAJITAKA MANGA


Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga ametembelea Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka Manga, kwa ajili ya Kukagua Maendeleo ya Mradi

Akielezea hatua ya Mradi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hosea Maghimbi amesema Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 1.73 umefikia asilimia 71 ya utekelezaji wake na Ujenzi wa Mabwawa matano ya kutibu majitaka umekamilika.

Amesema Mradi unatarajiwa kukamilika tarehe 27 Oktoba 2025 na Shughuli zinazoendelea kwa sasa, ni ufungaji wa fensi kuzunguka eneo la mradi, ulazaji wa mabomba ya kupitisha maji taka kati ya mabwawa na ukamilishaji wa Maabara ya kupima majitaka.

Dkt. Fatuma amepongeza hatua iliyofikiwa na kuelekeza SUWASA kuendelea kusimamia vyema Mradi huo, ili kufikia lengo la Mradi la kuhudumia wananchi kwa wakati uliopangwa.

Mradi huu unatarajia kuimarisha Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Singida, kuondoa hatari ya magonjwa ya kuhara na matumbo, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutoa maji yaliyotibiwa na mbolea bora.